Share news tips with us here at Hivisasa

Kiongozi wa wachuuzi na wafanyibiashara wadogo mjini Nakuru Simon Sangale Ole Nasieku amemtaka mratibu wa usalama katika kanda ya bonde la ufa Wanyama Musiambu kumpa usalama wa kutosha kwani anahofia maisha yake yamo hatarini.

Hayo yanajiri kufuatia shutuma alizotoa dhidi ya Gavana Kinuthia Mbugua kuhudhuria mazishi ya mkaazi mmoja wa Engashura na mwanabiashara wa Nakuru anayedaiwa kuwa mwanachama wa kundi la Mungiki wiki mbili zilizopita.

Katika kikao na wanahabari Jumatano mjini Nakuru, Ole Nasieku amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kwamba baada yake kukashifu hatua hiyo amekuwa akitumiwa watu nyumbani kwake kumtahadharisha.

“Tangu wakati ambapo nilikashifu hatua ya gavana Kinuthia kuhudhuria mazishi ya Jose ambaye alikuwa kiongozi wa Mungiki, nimekuwa nikipokea vitisho na sasa ninahofia hata familia yangu. Ninaomba bwana Musiambo achukue hatua ya haraka kuhakikisha kwamba maisha yangu yanalindwa, kwa sababu siku ya Jumamosi nilipokea wazee wawili nyumbani kwangu wakaniambia nijihadhari vile ninavyoongea mambo ya Mungiki na gavana,” alisema Ole Nasieku.

Wakati uo huo amesema kuwa hatatishwa na viongozi wachache wanaonuia kusambaratisha amani katika kaunti ya Nakuru na taifa kwa jumla.

“Ingekuwa ni vyema ningechukuliwa hatua za kisheria kuliko kunitisha kwa sababu nimechaguliwa kuwakilisha wanabiashara hapa Nakuru, siwezi nikanyamaza nikitetea wanabiashara na ukweli,” alisisitiza.