Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa Mombasa Hassan Omar alitangaza rasmi azma yake ya kuwania kiti cha ugavana wa Kaunti ya Mombasa siku ya Jumapili.

Licha ya kwamba yeye na Gavana wa Mombasa Hassan Joho wanatoka katika muungano mmoja wa kisiasa, Cord, viongozi hao wawili kwa muda wameonekana kutokuwa na misimamo sawa huku kila mara wakikosoana.

Akiongea katika mahojiano na radio moja siku ya Jumatatu, Seneta Omar alikosoa miradi ambayo Gavana Joho anaendeleza katika kaunti hiyo, kwa kudai kwamba ni njia tu ya kuwafumba watu macho.

“Joho anatengeza barabara fupi tu alafu anaweka picha yake hapo kuonyesha kuwa amefanya kazi lakini hakuna maendeleo yoyote aliyoleta Mombasa tangu serikali ya ugatuzi ilipoanza.” alisema Omar.

Seneta huyo alidai kuwa Joho hajatimiza ahadi ya kutengeza barabara katika eneo hilo na kuongeza kuwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika kaunti hiyo wanaogopa kufanya hivyo kutokana na ada ya juu wanayotozwa.

Mara kwa mara seneta huyo amekuwa akikosoa matumizi ya fedha katika kaunti ya Mombasa huku akitoa madai kuwa fedha za maendeleo zimekuwa zikitumika vibaya.

Omar anayewakilisha chama cha Wiper ameeleza kuwa nia yake ya kuongoza Mombasa kama gavana imetokana na jinsi anavyoona kaunti hiyo ikiendeshwa kwa njia isiyofaa.

Tangazo la Omar ambalo linaendelea kuibua hisia mseto kisiasa linakuja huku maseneta kadhaa humu nchini pia wakionyesha nia yao ya kugombea viti vya ugavana katika kaunti zao.