Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar amesema kuwa wawakilishi wadi katika bunge la kaunti hiyo wameshindwa kutetea haki za wananchi inavyostahili, kwa kukosa kuwa na misimamo dhabiti bungeni.
Omar alisema kuwa wengi wa wawakilishi hao wanaendesha kazi kulingana na maslahi ya viongozi wengine na sio wananchi waliowachagua kuwawakilisha bungeni.
Akiongea katika uwanja wa Caltex wilayani Likoni siku ya Jumapili, Omar alisema kuwa hakuna mwakilishi katika bunge hilo anayesimama wima na kuongea kulingana na mawazo yake bila kushawishiwa.
“Hakuna hata mwakilishi wadi mmoja pale anayeweza kusimama na kusema hapana. Sasa wewe uliletwa kuwakilisha wananchi ama kuwakilisha maslahi ya mtu binafsi?” aliuliza Omar.
Seneta huyo alisema hali hiyo imefanya serikali ya kaunti kulemaa na kubaki nyuma katika kutekeleza majukumu yake, jambo alilosema kuwa linatokana na utendakazi duni wa wawakilishi hao.
Wakati huo huo, Omar amewahimiza watu wa Mombasa kuhakikisha kuwa wanawachagua viongozi wapya kuwawakilisha katika bunge la kaunti, ili kuwaondoa wale waliopo sasa.
“Nawaambia wakaazi wa Mombasa kama mnataka kurekebisha uongozi wa kaunti lazima mbadilishe wabunge waliopo sasa kwa sababu suluhu hapa ni kuchagua watu wengine wapya,” aliongeza Omar.
Kiongozi huyo aliitaja hali hiyo kama ukiukaji wa katiba akisema kuwa viongozi wengi waliopo katika mamlaka hawafahamu kanuni za ugatuzi na serikali za kaunti jinsi zinavyofaa kuendeshwa.
Aidha, amewataja wabunge wa serikali za kaunti kama watu muhimu zaidi kuleta maendeleo kwa wananchi kwani ndio walioko karibu kabisa na wananchi ikilinganishwa na viongozi wengine.
Aliwahimiza wakaazi wa Mombasa kufanya uamuzi wenye busara ifikiapo wakati wa uchaguzi mkuu, mwaka ujao wa 2017.