Huku mchakato wa kisiasa ukizidi kuendelea katika Kaunti ya Mombasa, Seneta wa kaunti hiyo Hassan Omar amesema kuwa wananchi ndio watakaoamua kiongozi anayefaa kuchukua nafasi ya ugavana katika kaunti hiyo wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Akiwahutubia wakazi wa eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa siku ya Jumapili, Sarai alisema kuwa hakuna kiongozi atakayekubali kuwepo na kiti cha kupewa ama kukubali kuteuliwa kiongozi, bali lazima viongozi hao kuonyesha ubabe wao wa kisiasa.
Omar alidai kuwa uongozi unaotekelezwa kwa sasa katika kaunti ya Mombasa na Gavana Hassan Joho ni uongozi wa kiimla na kizamani, na kamwe hatahama mrengo wa Cord bali atasalia katika mrengo huo ili kubadili uongozi wa Kaunti ya Mombasa na taifa zima kwa jumla.
"Mimi nasema kuwa nitasimama kuwania kiti cha ugavana wa Mombasa na wananchi ndio watakaoamua ili tubadili uongozi wa Mombasa. Niko tayari kusimamia kidete kuhakikisha kuwa tumechukua serikali ya kaunti ya Mombasa,” alisema Omar.
Wakati uo huo aliwashauri wakaazi wa Kaunti ya Mombasa kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kuhusika kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao, na kuwachagua viongozi waadilifu ili kubadili uongozi wa taifa hili.
"Tunawasihi wakaazi wa Kaunti ya Mombasa kujisajili kwa wingi na kuwachagua viongozi wanaofaa kuongoza kaunti hii na serikali kuu, ili kuhakikisha kwamba mambo ya kudhulumiana hakuna tena,” alisema Omar.
Mchakato huo wa kisiasa umechukua mkondo mpya huku baadhi ya viongozi wa Kaunti ya Mombasa wakionekana kumezea mate kiti hicho, na kuahidi kuwatekelezea wananchi maswala muhimu ya kimaendeleo hasaa mashinani.
Viongozi waliyotangaza kuwania kiti cha ugavana wa Kaunti ya Mombasa katika uchaguzi mkuu ujao ni pamoja na Gavana wa kaunti hiyo Hassan Joho, Mbunge wa Nyali Hezron Awitti, Seneta wa Kaunti ya Mombasa Hassan Omar, na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Hazel Katana.