Afisa mkuu wa trafiki katika eneo la Bonde la Ufa Bi Mary Omari, amesema kwamba oparesheni inayoendelea dhidi ya magari ya uchukuzi wa umma katika eneo hilo, itaendelea hata baada ya wasafiri kupungua.
Hatua hiyo inalenga kupunguza idadi ya watu wanaopoteza maisha ama kujeruhiwa kufuatia ajali za barabarani, haswa kwenye barabara kuu ya Nakuru kuelekea Eldoret.
“Tunafanya oparesheni hii ili kuhakikisha kwamba magari yote ya usafiri wa umma yamo katika hali nzuri. Hatua hiyo itawazuia madereva kuendesha magari ovyo shule zinapofunguliwa,” alisema Omari.
Akizungumza siku ya Jumatatu, Bi Omari alisema kuwa maafisa wa trafiki wanashirikiana na wale wa mamlaka ya usafiri na usalama barabarani NTSA.
Alisema kuwa na maafisa hao wanashika doria katika maeneo mbalimbali ya barabara hiyo kuu, ili kunasa madereva wanaokiuka sheria za trafiki.
Katika muda wa siku tano, watu saba wameaga dunia kwenye barabara ya Nakuru-Eldoret, katika eneo la Salgaa, kwenye ajali mbili tofauti.
Watano waliofariki mkesha wa mwaka mpya walikuwa wanafunzi.