Mwakilishi wa wadi ya Sensi eneo bunge la Kitutu Chache Onchong’a Nyagaka amesema atawapunguzia mzigo wazazi ambao wanao watapata zaidi ya alama 300 katika matokeo ya mtihani wa darasa la nane ambayo yatatangazwa rasmi juma lijalo.
Kulingana na mwakilishi huyo, mwanafunzi yeyote atakayefikisha alama 300 na zaidi katika matokeo hayo atamfadhili kwa kumpa godoro na sanduku la vitabu anapojiunga na kidato cha kwanza mapema mwaka ujao.
Akizungumza na mwandishi huyu mnamo siku ya Jumatatu mjini Kisii, Nyagaka alisema aliamua kuwapunguzia wazazi mzigo kwa kufadhili wanao ambao matokeo ya mitihani yao ya darasa la nane.
Nyagaka aliahidi kuendelea kutoa usaidizi wa kielimu kuhakikisha kila mwanafunzi anapata masomo ili kujiendeleza kimaisha kupitia elimu.
Aidha, aliomba wazazi wote wa Kaunti ya Kisii kuwasomesha wanao ili kupokea elimu ambayo alisema ni silaha ya maisha haswa kwa kutafuta ajira nchini.
“Naomba kila mzazi kumsomesha mwanaye ili kupata elimu ambayo itamsaidia katika siku sijazo,” alisema Nyagaka.
“Katika maisha ya leo, hakuna mtu ataruhusiwa kuajiriwa ikiwa hana masomo ya kutosha. Naomba wale wako na tabia ya kuwaachisha wanao shule katika darasa la nane na katika kidato cha nne wakomeshe na kuwaendeleza hadi vyuo vikuu,” aliongeza.