Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa eneo bunge la Mugirango kusini kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kutabasamu baada ya gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae kuahidi kuanzisha ujenzi wa  kiwanda cha miwa katika eneo hilo.

Hii ni baada ya wakazi wa eneo hilo kuomba serikali hiyo kuwajengea kiwanda hicho ili kujiimarisha kibiashara,  kwani eneo hilo lina wakulima wengi wa miwa.

Akizungumza siku ya Jumanne katika soko la Riosiri eneo bunge la Mugirango kusini wakati soko hilo lilikuwa linafunguliwa rasmi, Ongwae alisema serikali yake imeimarisha mikakati yake ya kujenga kiwanda hicho, huku akisema hivi karibuni ujenzi wa kiwanda hicho utang’oa nanga rasmi.

“Kile ambacho kimekuwa kikituchelewesha kujenga kiwanda cha miwa hapa Mugirango kusini ni ukosefu wa shamba ambapo tungejenga, lakini hadi sasa kila kitu kiko shwari na ujenzi utaanza hivi karibuni,” alisema Ongwae.

”Najua eneo hili lina wakulima wengi wa miwa na mmekuwa mkipata hasara kwa kutokuwa na soko ya miwa kwa wakati mrefu, naomba muongeze kupanda miwa kwa wingi maana kiwanda kitakuwa eneo hili ambapo mtakuwa mnapeleka miwa yenu,” aliongeza Ongwae.

Wakati huo huo, Ongwae aliahidi kuweka miradi ya maji katika eneo bunge hilo ili wakazi kutosumbuka kwa ukosefu wa maji kwa kutembea safari ndefu.