Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amewaomba wawekezaji kuwekeza katika kaunti yake ili kufanya kazi pamoja na kuinua uchumi.
Kulingana na Ongwae, serikali yake iko tayari kufanya kazi na wawekezaji kuhakikisha kaunti yake imeinuka kimaendeleo na kiuchumi.
Ongwae alisema yeye kama gavana atatia sahihi na mwekezaji yeyote ambaye atawekeza kwa Kaunti ya Kisii, na kuongeza kuwa hiyo ndio njia mojawapo kaunti hiyo itainuka na kujiendeleza.
“Naomba tujiunge pamoja ili tuinue uchumi wa Kaunti ya Kisii. Wawekezaji mmekaribishwa kuwekeza maana kaunti yetu ina mazingira bora kwa biashara na serikali ya kaunti hiyo imejitolea kufanya kazi na wawekezaji kutoka nchi zote,” alisema Ongwae.
Wakati huo huo, Ongwae alisema serikali yake itajaribu kuhakikisha sekta ya afya imeimarishwa kikamilifu, ukarabati wa barabara umefanywa jinsi unastahili, na miradi ya maji imewekwa jinsi inavyostahili miongoni mwa mengine mengi.
Ata hivyo, Ongwae aliahidi kufanya maendeleo mengi zaidi katika kaunti hiyo kabla ya mwaka wa 2017 ili kutimiza ahadi alizotoa alipokuwa anatafuta kura katika uchaguzi uliopita.
Gavana Ongwae alikuwa anazungumza siku ya Jumapili kupitia redio ya Egesa, wakati wa mahojiano kuhusu maendeleo.