Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameombwa kuanzisha mashirika ya waendeshaji bodaboda katika kila sehemu ya kaunti hiyo ili kuwanufaisha wahudumu hao kibiashara na kuinua uchumi wa taifa
Kulingana na waendeshaji hao, pindi mashrika hayo yatakapoanzishwa yatawasaidia pakubwa haswa katika vikundi kwa kukabidhiwa mikopo ambayo itawasaidia kufanya biashara na kujiendeleza kimaisha na kuinua uchumi wa kaunti na wa kitaifa.
Wakizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumanne mjini Kisii, waendeshaji bodaboda hao, wakiongozwa na David Mogaka waliomba gavana Ongwae kuanzisha mashirika ili kuwasaidia waendeshaji hao kujinufaisha.
Pia walisema mikopo kwa wahudumu haswa wale hawana pikipiki zao ni muhimu kwani watanunua pikipiki zao kujifanyia biashara za uchukuzi badala ya kuendesha za wenyewe.
“Tukiwa na mashirika yetu yatatusaidia sisi vijana ili kujinufaisha katika maisha yetu. Tunaomba Gavana Ongwae atuanzishie mashrika yetu sisi wanabodaboda kando na kuhusishwa na vijana wengine,” alisema Mogaka.
Aidha, waliomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuzikarabati barabara zile hazipitiki ambazo ziko karibu na mji wa Kisii, huku wakitumia mfano wa barabara ya mjini Kisii-Nyamataro, Nyambera-Nyankongo, miongoni mwa zingine ambazo walidai ni mbovu ambazo wanahitaji zikarabatiwe ili kurahisisha biashara zao za uchukuzi.