Gavana wa Kaunti Kisii James Ongwae ameombwa kuharakisha ujenzi wa soko la Marani katika eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini ili kuimarisha biashara katika soko hilo.
Wafanyibiashara hao wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuharakisha kulikarabati soko hilo ambalo lilianza kukarabatiwa mapema mwaka jana, na hadi sasa halijakamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne, mwenyekiti wa wafanyibiashara wa soko hilo Bernard Ong’era alisema kuwa soko hilo linapaswa kukamilishwa haraka iwezekanavyo ili kuwe na mpangilio na utaratibu wa kuwasilishwa bidhaa na kuondolewa kwa mazao humo ndani kwani biashara havinogi kwa sasa.
Aidha, mwenyekiti huyo alisema kuwa imekuwa vigumu kwa watu kuhudumu katika soko hilo kwa shughuli za biashara, na kuongeza kuwa wafanyibiashara wamekuwa wakipanga bidhaa zao za kuuza hadi barabarani, hali ambayo inasababisha njia kufungwa na kuleta msongamano wa magari kila wakati
“Soko hili lilianzishwa kukarabatiwa lakini halijakamilika hadi sasa. Tunaomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuharakisha ujenzi wa soko hili ili ukamilike na wafanyibiashara kupata nafasi ya kufanya shughuli zao za biashara,” alisema Ong’era.
Pia mwenyekiti huyo alishangaa ni kwa nini ukarabati wa soko hilo umechukua zaidi ya miaka mitatu tangu awamu ya kwanza ya ukarabati huo kuanzishwa na kuachiwa njiani.
Mwenyekiti huyo aliitaka serikali ya Gavana Ongwae kuzuru soko hilo na kujionea matatizo ambayo wanapitia wanapotekeleza shughuli zao za biashara ili kujali mahitaji yao