Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameombwa kukarabati soko zote kwa njia ya kisasa kabla ya kualika wawekezaji kuwekeza katika kaunti hiyo.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa baadhi ya masoko katika kaunti hiyo yako katika hali ile ya zamani kabla ya serikali za ugatuzi kuanzishwa, haswa katika masoko yote yaliyopo mjini Kisii pamoja na ile ya Daraja Mbili.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Kisii, mwenyekiti wa wafanyibiashara katika kaunti hiyo Elijah Ombongi alisema itakuwa vizuri maendeleo kuonekana kutoka kiwango cha chini kabla ya kufikia kiwango cha juu zadi, na kusema gavana Ongwae sharti akarabati soko zote zilizopo mjini Kisii kwa njia ya kisasa kabla ya kualika wawekezaji.
“Lazima maendeleo yaanzie hapa chini, kumanisha soko zote sharti zikarabatiwe kwa njia ya kisasa ili wawekezaji wanapoalikwa wapate soko zetu ziko shwari,” alisema Ombongi.
“Soko la ‘Marketi’ lililoko katikati mwa mji wa Kisii, soko la eneo la St Judes, soko la Daraja Mbili na zingine zikarabatiwe kwa njia ya kisasa kwanza kisha baadaye wawekezaji wanapokuja wapate kila soko iko kwa njia ya kisasa na kupendeza,” aliongeza Ombongi.
Aidha, Ombongi na wafanyibiashara wengine waliomba Gavana Ongwae kutimiza ahadi alizotoa kwao alipotembelea wafanyibiashara hao mwezi wa nne mwaka jana kuwa angeweka mradi wa maji kwa masoko mjini Kisii kujenga nyua kwa masoko kuleta usalama na mengine mengi.