Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amepongezwa kwa kuagiza muda wa kurudisha fomu za basari kwa ofisi za wawakilishi wadi kuongezwa ili wanafunzi kupata fursa ya kujaza fomu hizo.
Hii ni baada ya gavana Ongwae kuagiza muda huo kuongezwa zaidi ili idadi kubwa ya wanafunzi kupata fursa wa kujaza fomu hizo na kufadhiliwa kimasomo.
Kulingana na Ongwae, ikiwa fomu hizo zitarudishwa kwa sasa basi huenda wanafunzi ambao wanajiunga na kidato cha kwanza wakakosa fursa ya kujaza fomu hizo.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumapili mjini Kisii, wazazi wengi walimpongeza Ongwae kwa uauzi huo.
Ongwae alisema hakuna haja wanafunzi wengine kufungiwa nje katika ufadhili wa masomo kwani pesa hizo zilitengwa na serikali ya kaunti kuwafaidi wanafunzi wote.
“Tunaona gavana wetu Ongwae anajali maslahi ya wanafunzi ili kupata masomo kupitia ufadhili na kuna wengine ambao hakuwa wamejaza fomu hizo,” alisema Benson Osoro, mzazi.
Aidha, Ongwae aliwataka washikadau wote wa elimu katika kaunti ya Kisii kushirikiana kuhakikisha viwango vya masomo vimeinuka.