Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amepongezwa kwa 'kujali maslahi' ya waendesha bodaboda wa kituo cha Marani kwa kuwajengea kibanda cha kujikinga na mvua inayoendelea kunyesha nchini na hata jua kali.
Waendesha bodoboda wa kituo hicho sasa wako na kila sababu ya kutabasamu baada ya kupata afueni kutoka kwa gavana Ongwae na serikali yake.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne mjini Marani, mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda wa kituo hicho Alfred Masira na wengine walimshukuru gavana kwa hatua hiyo.
Aidha waliongeza kuwa wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu, haswa wakati huu wa mvua nyingi ambayo inaendelea kunyesha kote nchini, na ambayo inadaiwa kuwa ya gharika.
"Tangu tuanze sekta hii ya uchukuzi tumekuwa tukisumbuka kwa kunyeshewa, wengine tukikimbia manyumbani maana hatukuwa na mahala pa kujikingia mvua inaponyesha," alisema Masira.
“Tunampongeza gavana wetu Ongwae kwa kutujengea kibanda hiki na tunamwomba aendelee kufanya maendeleo ya aina hiyo,” aliongeza Masira.
Kulingana na waendesha bodaboda hao, wameanza kufurahia matunda ya ugatuzi ambayo wengi wanasubiri kushuhudia kabla ya miaka mitano kukamilika katika Kaunti ya Kisii.
“Tumeona uzuri wa serikali za kaunti maana hatungekumbukwa kama sisi waendesha bodaboda, lakini ugatuzi umetuwezesha tumekumbukwa na tunafurahia kwa kiwango cha juu zaidi,” alisema Samson Makori, mwendesha bodaboda mwingine.
Ongwae ameombwa kuendelea kusaidia waendeshaji wengine ambao hawana vibanda hivyo.