Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae amewahimiza wakazi wa kaunti hiyo kutoa ushuru jinsi inavyostahili ili kutumika kufanya maendeleo.

Kulingana na Ongwe, ikiwa wakazi, haswa wafanyibiashara hawatatoa ushuru jinsi inavyostahili, hakutakuwa na maendeleo katika kaunti hiyo.

Akizungumza siku ya Jumanne katika mkahawa wa Ufanisi mjini Kisii, Ongwae aliomba wananchi wa kaunti hiyo kushirikiana na serikali ya kaunti hiyo kufanya maendeleo kwa kuchangia kupitia kulipa ushuru kikamilifu.

Ata hivyo, gavana huyo alisema kiwango cha ushuru kinachokusanywa katika kaunti hiyo kimerudi chini ikilinganishwa na hapo awali kwa kila mwaka, kufuatia ulipaji duni na hata wakusanyaji kutokusanya jinsi inavyostahili.

“Naomba wakazi wa kaunti hii kushirikiana na serikali yangu ya kaunti ili kuleta maendeleo katika kaunti yetu na wawe wanatoa ushuru jinsi inavyostahili ili pesa hizo kutumika kufanya maendeleo,” alisema Ongwae.

Wakati huo huo, Ongwae aliitikia mradi wa kukusanya ushuru kwa njia ya kielektroniki kuanzishwa katika kaunti hiyo ili iwe rahisi serikali kupata ushuru kikamilifu .

Inashukiwa kuwa baadhi ya wakusanyaji ushuru katika kaunti hiyo huwa wanatumia risiti mbili za kukusanya ushuru, huku kitabu kimoja cha risiti kikiwa chao binafsi na kingine kikiwa cha serikali.

“Mradi wa kuanzisha ushuru kupitia elekrtroniki ni jambo nzuri sana na mradi huo nimeukubali kuanzishwa kwa kaunti hii kwani tutapata ile ushuru yetu tunayostahili na kufanya maendeleo mengi,” aliongeza Ongwae