Mkurugenzi wa afya katika kaunti ya Kisii Geoffrey Ontomu amewashauri wakazi wa kaunti hiyo kufika katika hospitali mbalimbali za kaunti hiyo kupimwa ugonjwa wa ukimwi na kujua hali zao.
Kulingana na Ontomu, hakuna haja kwa wakazi kususia kupimwa ugonjwa huo kwani kujua hali ya kimwili kunasaidia pakubwa.
Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano mjini Kisii, Ontomu alisema ni mhimu kwa kila mtu kujitolea kujua hali yake ya kiafya, huku akitoa wito kwa kila mkazi kupimwa ugonjwa huo wa ukimwi.
“Ugonjwa wa ukimwi huwezi kuua mtu anapofuata taratibu zile zinazostahili, la kwanza ni kukubali ikiwa una virusi, kupunguza msongo wa mawazo, na kunywa dawa zile tunawapokeza,” alisema Ontomu.
“Naomba kila mtu afike kwa hospitali ili kupimwa ukimwi, mtu akipatikana na ugonjwa huo tutamuweka katika ratiba ya kupokea dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo ili kuendelea na maisha kama kawaida na kama watu wengine,” aliongeza Ontomu.
Ontomu aliomba wakazi kutoogopa kufika kwa mahospitali ila kujitolea kupimwa.
Wakati huo huo, aliomba watu kujikinga kuathiriwa na virusi hivyo wanapofanya ngono, huku akiongeza kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamerudi chini katika kaunti ya Kisii kwa mwaka mmoja sasa ikilinganiswha na miaka mingine iliyopita.