Daktari mkuu katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Kisii Geoffrey Ontomu amesema viwango vya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi katika kaunti ya Kisii vimepanda hadi asilimia nane.
Hii ni baada ya ukahaba kuongezeka zaidi katika mji wa Kisii, jambo ambalo limeonekana kupandisha viwango vya maambukizi hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika hospitali hiyo mjini Kisii, Ontomu alisema maambukizi hayo yamepanda huku akiomba wananchi kujihadhari zaidi ili kutokabiliwa na ugonjwa huo.
Mnamo siku ya Ijumaa wiki jana, makahaba zaidi ya 300 walitiwa mbaroni mjini Kisii kwa kupatikana na kosa la kufanya ukahaba, wengi wakiwa wajawazito, chini ya miaka 18 kulewa zaidi miongoni mwa makosa mengine
Makahaba hao pia walilazimika kupimwa katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Kisii kujua hali zao na ikabainika wengi wako na ugonjwa na wengine wajawazito.
Kaunti ya Kisii ni kaunti ya wita kwa kuwa na idadi nyingi ya watu ambao wameathirika na ugojwa wa ukimwi, huku ikiwa na zaidi ya watu 70,000 ambao wameathiriwa na ugonjwa huo, hayo ni kwa mujibu wa Ontomu.
Ontomu aidha aliongeza kuwa bidhaa vya kupima ugonjwa wa ukimwi vimeisha, na kulazimika kusimamisha shughuli ya kupima ugonjwa huo kwa muda hadi serikali kuu itume vifaa hivyo kwenda kwa kaunti hiyo.
“Kaunti ya Kisii imeonekana kupandisha viwango vya maambukizi ya ukimwi. Naomba watu kujiadhari zaidi na kulinda maisha yao, kwa sasa viwango hivyo vimepanda hadi asilimia nane, jambo la kushangaza sana,” alisema Dkt Ontomu.
"Naomba serikali ya kitaifa kutuma bidhaa na vifaa vya kupima ugonjwa huo wa ukimwi kwani tumekuwa na upungufu, na tumesimamisha shughuli ya kupima ukimwi hadi serikali kuu itume bidhaa hivyo,” aliongeza.