Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josephine Onunga amewaonya madereva wa magari pamoja na waendeshaji pikipiki dhidi ya kutokuwa waangalifu barabarani kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kulingana na Onunga, visa vya ajali vimekuwa vikiongezeka barabarani kufuatia madereva na wanabodaboda kutokuwa waangalifu wanapofanya biashara zao za uchukuzi, na kusema yeyote atafumaniwa akivunja sheria za barabarani atachukuliwa hatua za  kisheria.

Onunga alisema visa vya ajali vitapungua ikiwa madereva na wanabodaboda watafuata sheria za barabarani kila wanapofanya biashara zao za uchukuzi.

Akizungumza mnamo siku ya Jumanne mjini Nyamira, Onunga aliwataka madereva hao na waendeshaji bodaboda kuwa waangalifu na kufuata sheria za barabarani ili kupunguza visa vya ajali.

Onunga alisema tangu mwaka huu wa 2016 uanze,  visa vya ajali vimeongezeka kati ya Kaunti za Kisii na Nyamira.

Mnomo siku ya Jumatatu, gari aina ya Nissani lilihusika katika ajali eneo la Omosocho katika barabara ya Nyamira-Kisii, huku ajali nyingine ikifanyika siku hiyo hiyo katika eneo la Gesenero, ajali ambazo ziligharimu maisha ya watu watatu kufikia sasa.

“Naomba madeva kuwa waangalifu barabarani kwani maisha ya binadamu ni ya muhimu sana, sharti kila mtu awe anafuatilia sheria za barabarani," alisema Onunga.

"Na wale wa kuendesha bodaboda naomba nao waweze kufuata sheria hizo ili tupunguze visa vya ajali,” aliongeza Onunga.