Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mkurugenzi wa mazingira katika kaunti ya Kisii Samson Bokea amewaonya vikali wakazi wa kaunti hiyo wanaotupa uchafu kiholela kwa maji ya mito mbalimbali kuchafua mazingira na kusema yeyote atafumaniwa atatoa faini ya shilingi 350,000.

Hii ni baada ya kubainika kuwa maji ya mito mingi katika kaunti hiyo ya Kisii huchafuliwa na wakazi ambao wanadaiwa kutupa uchafu kwa mito, kuoshea nguo kwa mito, kuogea kwa mito na kufungulia uchafu wa choo na kuchafua maji yanayopita katika sehemu mbalimbali za kaunti hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano afisini mwake Bokea alitoa tahadhali kwa wale walio na tabia hiyo na kusema siku zao zimehesabiwa kwani hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayefumaniwa akifanya makosa hayo.

“Naomba wale wamezoea kuchafua maji ya mito kujitenga na tabia hiyo na yeyote atafumaniwa akichafua mazingira atapigwa faini ya shillingi 350,000 ili kuwa funzo kwa wengine,” alisema Samson Bokea mkurugenzi wa mazingira Kisii.

Wakati uo huo, mkurugenzi huyo aliomba wakazi wa kaunti hiyo kushirikiana pamoja kulinda mazingira kwani mazingira ni uhai ili kuzuia magonjwa ambayo yanatokana na uchafu.