Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Ilibidi polisi wa utawala kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya watu ambao walishambulia askari mmoja katika kivuko cha feri cha Likoni na kumuumiza vibaya siku ya Jumanne.

Hii ni baada ya kujaribu kuwazuia watu ambao walikuwa wakiruka ukuta kukimbilia feri ambayo ilikuwa inapakiza watu na kuwavusha kuelekea katika ng’ambo ya pili.

Askari huyo ambaye anahudumu kwenye kivuko hicho kutoka kampuni ya kutoa usalama ya kibinafsi ya Texas alijipata kwenye hatari baada ya wakazi kuanza kuruka kuta za mabanda na kupita barabara za kutumiwa na magari na kwenda kwa nguvu, ambapo askari huyo na wenzake walijaribu kuwazuia watu ambao walikuwa na hasira kwa kucheleweshwa na feri.

Kulingana na Rose Oganga, ambaye alishuhudia kisa hicho, watu walikuwa tayari wamecheleshwa kwa zaidi ya saa moja kwenye kivuko hicho kufuatia feri moja kukwama katika eneo la ardhi, na walimwona askari huyo kuwa kikwazo kwao na kuanza kumchapa alipokuwa akiwasukuma na kutumia rungu yake kuwapiga baadhi yao.

“Askari huyo aliokolewa na maafisa wa polisi baada ya mmoja wao kufyatua risasi hewani na kuwatawanya watu waliokuwa wanampiga kwa mateke na wengine kutumia rungu lake,” alisema shuhuda huyo.

Mmoja wa maafisa wa feri hiyo alidokezea kuwa shida ilianza baada ya feri moja kukwama kwenye eneo la maegeshoni ambapo hutumiwa na feri nyingine kupakua na kupakiza watu na magari, ambapo ilikuwa shida feri mbili kuegesha kwa wakati mmoja.