Polisi mjini Molo wanawasaka wanaume watatu kwa tuhuma za kuteka nyara mwanafunzi wa darasa la nane kwa lengo la kumdhulumu kimapenzi.
Msichana huyo Mary wanjiru ameeleza wanahabari kwamba wanaume hao watatu walimfikia njiani alipokuwa akielekea shule ambapo walimsimamisha huku wakidai walikuwa na nia ya kuzungumza naye.
Alisema kwamba wanaume hao waliokuwa wamejifunika nyuso zao walimbeba kwa nguvu hadi kichakani na kumpatiliza kichapo kikali huku wakijaribu kumbaka.
Alisema juhudi zake za kupiga kamsa zilaambulia patupu baada ya mmoja wa watesi wake kumfunga mdomo huku akitishia kumuua.
“Nikiwa kwenye harakati za kujinasua, wanaume hao waliingiwa na hofu baada ya kuona mkulima mmoja akielekeza mifugo wake karibu na hapo na ndipo wakahepa na kuniacha nikilia kwa hofu na uchungu baada ya kunitesa kwa zaidi ya saa mbili,” msichana huyo alisema.
Habari za tukio hilo zilisambaa haraka katika eneo la Mianzini huku wakazi pamoja na waalimu wakifika na kuanza kuwasaka wahalifu hao watatu.
Babake mtoto huyo Ayub Wainana ameitaka idara ya polisi mjini Molo kufanya uchunguzi wa kina na kuwachukulia hatua kali za kisheria washukiwa ili kupunguza hofu ambayo inaendelea kutanda kuhusiana na usalama wa wanafunzi wa shule za kutwa ambao hurauka mapema kuelekea shuleni.
“Mwanangu anahitaji ushauri baada ya kuteswa japo alipokea matibabu katika hospitali ya wilaya ya Molo, lakini ana wasiwasi kuhusiana na usalama wake kwa wakati huu,” Wainaina alisema.