Mwenyekiti wa chama cha kupambana na dawa za kulevya katika Kaunti ya Kisii ambaye pia ni Mchungaji wa Chuo Kikuu cha Kisii kasisi Lawrence Nyaanga amedai kuwa baadhi ya maafisa wa polisi na machifu hushirikiana na wagema kuendesha biashara hiyo ya upikaji wa pombe haramu.
Kulingana na Nyaanga, maafisa wa polisi na machifu hupokezwa pesa wanapowafumania wagema, huku wagema hao wakiruhisiwa kuendesha biashara zao kama kawaida.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Kisii, Nyaanga aliomba maafisa wa polisi na machifu kujitenga na tabia hizo na kushirikiana kupunguza upikaji wa pombe haramu kwani pombe hiyo inaendelea kuathiri afya za watu wanaopugia pombe hiyo.
“Tunajua kuna baadhi ya maafisa wa polisi na machifu ambao huchangia kuendelea kwa upikaji wa pombe haramu katika vijiji mbalimbali kwa kupewa pesa,” alisema Nyaanga.
“Naomba mwe mstari wa mbele tupunguze pombe hiyo kwani ikiendelea kutengenezwa wengi wa wakazi wanaopugia afya zao zitadhoofika,” aliongeza Nyaanga.
Wakati huo huo, Nyaanga aliomba mahakama kuwachukulia hatua kali ya kisheria yeyote atafikishwa mahakama dhidi ya upikaji wa pombe ili kuwa funzo kwa wengine.
Aidha, aliomba wakazi kupiga ripoti ikiwa kuna mgema anapika pombe karibu nao ili wachukuliwe hatua za kisheria.