Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi mjini Nakuru wamelaumiwa pakubwa na wakaazi wa mtaa wa Bondeni viungani mwa mji huo, kwa kufyatua risasi kiholela na kumuumiza msichana mmoja wakati wa msako wa walanguzi wa dawa za kulevya Jumatano.

Wakaazi hao walisema risasi hiyo ilipenya nyumba ya mama mkwe wake mwadhiriwa kwa jina Becky Siongi mama ya mtoto mmoja, na kumpata mkononi.

Kulingana na mamake, Becky alikuwa akimpeleka mwanawe wa mwaka mmoja kulala, alipomwita akidhania amegongwa na stima.

“Hatukuwa tumeskia risasi yoyote na aliniita akiniambia ‘mama, nimegongwa na stima’. Tukachukua watoto kutoka nje, kufika kwa mlango nikaona anatokwa na damu mkononi na tulipomkagua tukaona ni risasi imempata,” mama huyo alisema.

Hata hivyo walisema waliendelea kusikia milio ya risasi, ambapo walisema haijakuwa mara ya kwanza kwa polisi kuvaamia eneo hilo na kuwahangaisha.

Naye Juliet Wanja, alisema: “Nilikuwa hapo nje nikasikia risasi zikilia na nilipoangalia nikaona polisi wakipiga risasi juu.”

“Wakitaka mtu waje washike mhalifu mwenyewe lakini si kutuumizia watoto, sasa tungekuwa tunalia maafa, hiyo risasi ingemuua huyo msichana ama mtoto wake,” Mary Wanjiku alisema.

Wakaazi hao walitaka polisi kuelekeza nguvu za kupigana na silaha kwa wahalifu na magaidi wa Al-shabab, badala ya kujeruhi raia wasio na hatia.

Mamlaka ya polisi mjini Nakuru ikiongozwa na OCPD Musa Kongoli, hawajasema lolote kuhusiana na tukio hilo la jioni ya Jumatano.

Hata hivyo Becky alikimbizwa na polisi hao katika hospitali kuu ya mkoa ya bonde la ufa mjini nakuru ili kuondolewa risasi iliyokuwa imekwama mkononi mwake.