Polisi wawili wanaodaiwa kumua marehemu Kwekwe Mwandaza wametilia shaka ushahidi wa mashahidi 19 uliotolewa dhidi yao na kuutaja ushahidi huo kama wa uwongo.
Kupitia wakili wao Cliff Ombeta, waliiambia mahakama siku ya Jumatano kuwa ushahidi huo hauambatani na sio dhihirisho kuhusiana na kesi hiyo.
Ombeta aliongeza kuwa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma haikuwasilisha leso iliyokuwa na damu ambayo ilitajwa kwenye ushahidi huo.
Aidha, alighadabishwa kwa nini askari wengine 11 waliokuwa kwenye oparesheni hiyo hawakufunguliwa mashtaka wala kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo.
Madai haya yalipingwa vikali na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Alexendra Muteti kwa kusisitiza kuwa uchunguzi uliofanywa ulidhihirisha kuwa wawili hao ndio walihusika kwenye mauwaji hayo, baada ya ripoti kutoka kwa msajili wa silaha katika kituo cha Kinango Adan Shora kuonyesha kuwa Veronica na Issa walitumia risasi 5 kwenye makabiliano hayo.
Aidha, Muteti aliongeza kuwa mchunguzi wa kibinafsi Emily Adhiambo alithibitishia mahakama kuwa kichwa cha mwendazake Mwandaza kilikuwa na mashimo ya risasi, ishara tosha kuwa alishambuliwa kwa bunduki.
Muteti ameitaka mahakama kuwachukulia hatua za kisheria wawili hao mara moja ili iwe funzo kwa maafisa wengine wa polisi wanaotumia silaha zao vibaya.
Aprili 23, 2014 wadogo wa Kwekwe waliiambia mahakama kuwa walilazimishwa kupiga magoti juu ya damu ya dada yao baada ya kupigwa.
Mahakama kuu inatarajiwa kutoa uamuzi Novemba 10 mwaka huu iwapo wawili hao wana kesi ya kujibu kabla ya kuhukumiwa.
Mnano Agosti 21, 2014 afisa wa polisi veronica Gitahi pamoja na Issa Mzee wanadaiwa kumpiga risasi mtoto huyo wa miaka 14 katika eneo la Maweu huko Kinango kaunti ya Kwale.