Polisi katika eneo la Eldoret mashariki leo hii Jumatatu wamefanikiwa kuzima kundi la wezi ambao wamekuwa wakishiriki katika visa vya wizi wa vifaa vya nyumba katika mtaa wa Kapsoya na mitaa mingine jirani.
Afisa mkuu wa polisi katika kituo cha polisi cha Eldoret mashariki Nelson Daliti alisema ufanisi huo umechangiwa na mpango wa nyumba kumi.
“Kundi hili limekuwa kero kwa wakazi wa mtaa wa Kapsoya kwa muda mrefu, tunashukuru wananchi kupitia kwa mpango wa nyumba kumi ambao umetuwezesha kukabiliana na mtandao wa kundi hili,” alisema Daliti
Akihutubia wanahabari afisini mwake, Daliti alisema vifaa ambavyo washukiwa hao walipatikana navyo ni tarakilishi, runinga, redio, mitungi ya gesi, miongoni mwa vifaa vingine.
Daliti alitaka wakazi wa mitaa husika kufika katika kituo cha polisi na kutambua mali yao ambayo alisema ni mali ya thamani takribani shilingi nusu milioni.
Washukiwa wawili ambao walinaswa na vifaa hivyo tayari wamefikishwa mahakamani mjini Eldoret.
Wakati huo huo, afisa huyo alisema idara ya usalama katika eneo hilo imeimarisha usalama msimu huu wa sherehe za Krisimasi na mwaka mpya, ambapo aliwataka wananchi kushirkiana na viongozi wa mpango wa nyumba kumi kutoa ripoti muhimu kuhusiana na wahalifu.
Afisa huyo alisema maafisa zaidi wataongezwa katika maeneo ambayo yanashukiwa kuwa hatari kwa usalama msimu huu wa sherehe.