Maafisa wa Polisi mjini Keroka wameombwa kuimarisha usalama mjini humo kufuatia kudorora kwa usalama katika siku za hivi maajuzi.
Hii ni baada ya naibu chifu wa lokesheni ya Nyasore wilayani Masaba kaskazini kaunti ya Nyamira Nyakego Bosire kushambuliwa na washukiwa wa ujambazi usiku wa kuamkia Jumapili.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili mjini Keroka, chifu wa Keroka Kennedy Ndege aliomba maafisa wa polisi kuimarisha usalama mjini humo pamoja na viungani mwake ili kupunguza visa vya wananchi kushambuliwa kila mara.
“Tunaomba maafisa wa polisi kuimarisha usalama katika mji wa keroka na sehemu zingine kwa kupiga doria nyakati za usiku ili visa vya mashambulizi kupunguzwa,” Kennedy Ndege alisema.
“Naibu chifu wa lokesheni ya Nyasore alishambuliwa na washukiwa wa ujambazi na alijeruhiwa vibaya na hii si mara ya kwanza visa vya utovu wa usalama vinaripotiwa hapa Keroka tunaomba usalama uimarishwe kikamilifu,” Ndege aliongeza.
Wakati huo huo , chifu huyo aliomba wananchi wote kushirikiana na maafisa wa polisi kuhakikisha kuwa kuna usalama wa kutosha kila sehemu ya kaunti ya nyamira.