Maafisa wa polisi wilayani Manga wameombwa kufanya uchunguzi na kuwatia mbaroni washukiwa ambao huwavamia na kuwajeruhi wanafunzi wa shule wanapoelekea shuleni asubuhi na mapema kila wakati.
Hii ni baada ya mwanafunzi mmoja wa kidato cha nne wa shule ya upili ya Ogango kufahamiwa leo Jumanne alipokuwa anaelekea shuleni na kudungwa kisu tumboni.
Akizungumza siku ya Jumanne baada ya kisa hicho, mwenyekiti wa shule hiyo ya upili Nyanga’au Ong’ondi alisema mwanafunzi huyo aliyejeruhiwa ni wa pili katika shule hiyo, huku akisema visa hivyo vimekuwa vikiendelea na washukiwa ambao hawajulikani.
Kisa hicho kilitibithishwa na chifu wa lokesheni ya Central Kitutu Evans Nyang’au ambaye alisema kijana huyo aliyemvamia mwanafunzi huyo tayari ametiwa mbaroni.
“Tunaomba uchunguzi ufanywe ili kikundi cha vijana ambacho kinavamia wanafunzi wanapoelekea shuleni waweze kukamatwa wote,” alisema Ong’ondi.
Visa vya aina hiyo vimekuwa vikishuhudiwa kila wakati katika kaunti ya Nyamira, huku maafisa wa polisi wakiombwa kutoa msaada ili kuokoa maisha ya watu.