Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi wameombwa kushirikiana na machifu wanapomwaga pombe haramu vijijini katika Kaunti ya Kisii.

Ombi hilo limetolewa baada ya afisa mmoja wa polisi kujeruhiwa vibaya wakati msako wa pombe haramu ulikuwa unafanywa katika kijiji na Boisanga Nyanchwa mapema wiki hii.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano mjini Kisii, mchungaji wa Chuo Kikuu cha Kisii ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha kupambana na dawa za kulevya katika Kaunti ya Kisii kasisi Lawrence Nyaanga alikashifu kitendo cha afisa wa polisi kujeruhiwa.

“Ni vizuri kwa maafisa wa polisi kujulisha machifu kuwa siku fulani watafanya msako wa pombe katika kijiji fulani ili kuzuia kujeruhiwa kila mara,” alisema kasisi Nyaanga.

“Na wale ambao walimpiga afisa wa polisi, hiyo ni kukiuka sheria kwani maafisa wa polisi ni wa kuleta usalama na uchunguzi unaendelea ili aliyempiga afisa wa polisi kujulikana na kuchukuliwa hatua za kisheria,” alliongeza Nyaanga.

Aidha, Nyaanga alisema pombe haramu haitaruhisiwa kuendelea kuuzwa katika Kaunti ya Kisii, na kusema msako wa kumwaga pombe hiyo hautakomeshwa hadi wagemaji wakomeshe hulka hiyo.