Maafisa wa polisi, Nyamira wameombwa kufanya uchunguzi dhidi ya watu ambao wanazikata nyaya za stima na kuharibu transfoma katika eneo la Mongori Borabu, inayosababisha ukosefu wa nguvu za umeme katika eneo hilo.
Wito huo umetolewa na wakazi wa eneo hilo baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya watu wanaoshukiwa kukata nyaya za stima kunapokuwa usiku na kuwaacha kwa giza.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne katika eneo la Borabu, Elijah Mogonga aliyeongea na waandishi kwa niaba ya wakaazi wengine alisema kuna baadhi ya wezi ambao hukata nyaya za umeme na kuharibu transfoma wakati wa usiku inayosababishia ukosefu wa nguvu za umeme kila wakati.
Wakaazi hao wameomba maafisa wa polisi kuanzisha uchunguzi na kuwatia mbaroni wezi hao kwani wamekuwa wakisumbuka kupita kiasi.
Wakaazi hao tayari wamewasilisha malalamishi yao kwa kampuni ya usambazaji umeme KPLC huku wakiiomba ishughulikie swala hilo.
“Kuna watu ambao hukata nyaya za stima na kutuacha kwa giza .Tunaomba maafisa wa polisi kuanzisha uchunguzi na kuwatia mbaroni wahusika hao na tayari tumepiga ripoti kwa kampuni ya usambazaji umeme KPLC,” alisema Elijah Mogonga.