Share news tips with us here at Hivisasa

Polisi wa kituo cha Bahati walifanikiwa kutibua njama ya wezi waliokuwa wamejihami kwa bunduki siku ya Jumanne, waliovamia boma la mwanabiashara mmoja katika eneo la Ahero, wadi ya Bahati, kaunti ya Nakuru.

Wezi hao ambao idadi yao haijulikani hadi sasa walikuwa na gari aina ya Nissan walipovamia boma la mwanabiashara huyo karibu na boma la meneja wa CDF ya Bahati mwendo wa saa sita usiku.

Hata hivyo, baada ya kupiga kamsa, wananchi walijulisha polisi kuhusu uhalifu huo ambao waliitikia wito huo na kwa ushirikiano na mwenyekiti wa wanabiashara wa Ahero Rafael Mwangi na vijana wengine wanne wakafuata wezi hao huku wakifyatuliana risasi.

Wezi hao walizunguka katika barabara za kijiji hicho huku wakijaribu kukwepa polisi, hadi wakatokea barabara kuu ya Nakuru-Nairobi eneo la section 58 ambapo polisi hawangeweza kuwafuata tena.

"Tuliwakimbiza tukijihadhari kwa kuwa tulikuwa na watu ambao ni raia na walipiga risasi tatu wakituelekezea, na kutulazimisha kujibu. Hakuna aliyejeruhiwa," akasema afisa mmoja aliyeomba kubanwa jina.

Uhalifu huo unajiri baada ya mwanabiashara mwingine kuuawa kwa kupigwa risasi na wezi siku moja kabla ya krisimasi.

Mkazi mmoja ambaye alikuwa akizungumza na mwandishi huyu katika eneo hilo aliitaka serikali kuwalipa viongozi wa nyumba kumi ili wapate bidii zaidi ya kukabiliana na uhalifu.

Naibu kaunti kamishna katika kaunti ndogo ya Bahati Kithinji Ithai amedhibitisha hayo akisema uhalifu umeanza kuchipuka upya eneo hilo lakini watafanya doria zaidi.

Walisema hayo baada ya kufanya mkutano wa kiusalama katika eneo hilo na wakaazi.