Maafisa wawili wa polisi waliofutwa kazi kwa kuzuia msafara wa rais kupita eneo la Sabasaba mjini Mombasa wanapanga kwenda mahakamani kupinga jambo hilo.
Koplo Barnaba Rutto na afisa Joel Atuti wanadai madai hayo ni uzushi tu, wala wao hawakuhusika katika kutatiza msafara wa rais hivyo basi wakili wao ataishtaki tume ya huduma kwa polisi.
Wawili hao wanasema Januari 10,2016 walisimamisha gari lao mbele ya matatu iliyokuwa imesimama kati kati ya barabara eneo la Saba Saba ili kumshika dereva kwa kutatiza shughuli za barabarani.
Lakini katika hali hiyo ndio msafara wa rais ukafika na kutatizika, baada ya hapo walinaswa na siku tano baadaye kupewa barua za kufutwa kazi.
Wawili hao wanadai hawakuwa na taarifa kuwa barabara hiyo ingetumika na msafara wa rais.
Siku ya Jumamosi, rais Uhuru Kenyatta jijini Nairobi akizungumza kuhusu tukio hilo alisema aliona maafisa hao wawili wakichukua hongo.
Ni kutokana na kauli hii ndio maafisa hao wawili wanadai mashtaka yanayotumiwa kuwafuta kazi hayaeleweki na hakuna ukweli wowote.