Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Licha ya baadhi ya wananchi katika mji wa Nakuru kufurahia hatua ya tume ya kudhibiti kawi ya kupunguza bei ya mafuta ya taa pamoja na ile ya petrol na dizeli, madereva kwa upande wao wameonyesha kutoridhishwa kwao na hatua hiyo.

Baadhi ya madereva waliozungumza na mwandishi huyu mjini Nakuru siku ya Jumanne walidai kuwa hatua hiyo haitaleta mabadiliko yeyote katika sekta ya usafiri wa umma, na haswa kwa wale wanaotumia mafuta ya petroli ambayo imepunguzwa kwa senti 40.

Badala yake, madereva hao wameitaka tume hiyo ya kudhibiti kawi ERC kupunguza bei hiyo hata zaidi ili waweze kuzingatia ombi la wateja wao la kupunguza nauli hasaa wakati huu ambapo wakenya wanapitia hali ngumu ya maisha kutokana na ongezeko la gharama ya maisha.

"Shilingi moja ni kiwango kidogo sana ERC kupunguza kwa bei ya mafuta. Hatujafurahia hatua hiyo kwa kuwa gharama ya matumizi ya mafuta itasalia kuwa kama ile ya hapo awali. Ingawa bei ya petroli imepunguzwa kwa shilingi moja, hatutapunguza nauli, itasalia kuwa ile ya kawaida," alialama mmoja wa madereva mjini Nakuru kwa jina la Allan Kinuthia.

Kuhusiana na swala la iwapo nauli itaongezwa wakati ambapo watu watasafiri kuelekea mashambani wakati wa sikukuu ya krismamsi, madereva wa Nakuru wanaojihusisha na usafiri wa umma wamesema kuwa idadi ya watu ndio itakayotegemea iwapo watachukua hatua hiyo au la.

Kulingana nao, ongezeko la abiria litawapelekea kuongezea nauli kwani kutakuwa na upungufu wa magari ya usafiri wa umma, huku hitaji la usafiri likiwa juu.

Isitoshe, amesema wataongeza nauli hiyo kwani kwa kawaida wao hushuhudia idadi ndogo ya wateja wanaporejea kutoka safari hizo za mashambani na kutoana na hilo, hatua ya kuongeza nauli huwasaidia kupunguza hasara.

Kwa muujibu wa orodha ya bei mpya za mafuta iliyotolewa na tume ya kudhibiti kawi nchini ERC, bei ya dizeli imepungua kwa shilingi moja na senti 40, bei ya petrol imepungua kwa senti 40 huku ile ya mafuta ya taa ikipungua kwa shilingi moja na senti 54.

Bei hizo mpya zitatumika kuanzia Jumatatu hii ya tarehe 14 Desemba hadi tarehe 14 Januari mwaka ujao wa 2016.