Kiongozi wa muungano wa upinzani Raila Odinga ameendeleza shutuma zake dhidi ya serikali ya Jubilee kwa kuwataka viongozi wakuu wa serikali kuheshimu ahadi walizotoa kwa wananchi na kuhakikisha kuwa wanazitimiza zote.
Kiongozi huyo alishangaa ni kwa nini serikali hiyo bado inaendelea kutetea visa vya ufisadi ambavyo alisema vimekuwa vikienea kwenye idara pamoja na wizara mbali mbali za serikali tangu serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kuchukua hatamu za uongozi.
Akiongea katika eneo la Nyali kwenye hafla ya kuzindua jina la barabara moja ambayo imepewa jina la mwanawe Fidel Odinga, Raila alitaja visa vingi vya ufisadi kama vile vya Euro, ambapo alisisitiza msimamo wake kuwa serikali sharti iwajibikie visa hivyo na kujitokeza wazi kulishughulikia suala hilo.
“Sisi tulisema ufisadi kuhusu NYS na serikali ikanyamaza, sasa kuna Euro Bond, lazima serikali iwajibikie pesa za umma,” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo ambaye aliwahutubia wenyeji kwenye mitaa mbali mbali katika kaunti hiyo alisema kuwa ataendelea kuwawajibisha viongozi wa serikali ili kuona kuwa ahadi zote walizowapa wakenya zinatimizwa kikamilifu.
Waziri mkuu huyo wa zamani alikuwa amendamana na viongozi mbali mbali kutoka kaunti ya ya Mombasa pamoja na maafisa wakuu wa muunganao huo wa Cord na ziara hii inakuja siku chache tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukamilisha ziara yake.