Kinara wa Mrengo wa CORD Raila Odinga amekashifiwa vikali na baadhi ya wafuasi wake wa Cord wanaodai kuwa kukosa kuunga mkono serikali ya Jubilee inaponuia kufanikisha agenda za maendeleo kwa wakenya.
Kulingana na Mwakilishi wa Wadi ya Watamu Ibrahim Matumbo, Raila alionekana akiikosoa agenda ya serikali na kujitafutia umaarufu wa kisiasa hali ambayo inachangia pakubwa kuwepo kwa uhasama wa kisiasa.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumapili, baada ya kukutana na viongozi wa chama cha Jubilee, Matumbo alisema kuwa alihama rasmi mrengo wa Cord na kujiunga na Jubilee.
Matumbo aliwalaumu vinara wa CORD kwa kumteua Willy Baraka Mtengo kama mgombea wa kiti cha ubunge eneo bunge la Malindi kwenye uchaguzi mdogo.
MCA huyo aidha alimtaja Willy Baraka Mtengo kama anayekabiliwa na sakata za dhulma za kijinsia na unyanyasaji na kusema kuwa hafai kujiunga na kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi huo mdogo.
“Sidhani kama Willy Baraka Mtengo anafaa kuwania kiti hicho kwa sababu anakabiliwa na sakata nyingi sana za dhulma za kijinsia na unyanyasaji,” Matumbo alisema.
Wakati huo huo Matumbo aliunga mkono hatua ya serikali kuu kuzifunga kampuni za familia ya gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho hivi majuzi kwa madai ya kukosa kulipa ushuru akiitaja kuwa hatua hiyo ni njia moja wapo ya kukabiliana na ufisadi uliokita mizizi katika taifa hili.