Kiongozi wa muungano wa upinzani Cord Raila Odinga ameombwa kujitokeza na kuomba msamaha Jamii ya Gusii kwa kumuhusisha mwenyekiti wa Banki Kuu Mohammed Nyaoga kwenye sakata ya utumizi mbaya wa pesa za Eurobond.
Nyaoga anatoka Jamii ya Gusii na baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa wale ambao walitumia vibaya pesa hizo za Eurobond, jambo hilo limeibua hisia mbalimbali.
Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Kisii, mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Chache Kaunti ya Kisii Richard Tong’i alimuomba Odinga kuomba Jamii ya Gusii msamaha kwa kuhusisha mmoja wa Jamii hiyo kwenye utumizi mbaya wa pesa za Eurobond bila ushahidi.
Ata hivyo, Tong’i amesema ikiwa Raila Odinga yuko na ushahidi aweze kuwasilisha ili ukweli ubainike na kuacha kutaja watu ambao hana uhakikika kwa kuhusika kwenye sakata hiyo.
“Katika siku za hivi maajuzi kiongozi wa Cord Raila Odinga ameonekana kukemea ufisadi nchini lakini jinsi ameonekana kufanya mambo hayo sio njia ya kufurahisha maana amehusisha mmoja wa Jamii yetu kwenye sakata hiyo bila ushahidi wa kutosha,” alisema Tong’i.
“Naomba Odinga kujitokeza wazi na kuomba Jamii yetu ya mkisii msamaha kwa lile alilolifanya kwa kuhusisha mmoja wetu bila ushahidi," aliongezea Tong’i.