Kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani Cord, Raila Odinga, amewataka wenyeji katika eneo zima la Pwani kupuuza kugawanywa na waasi wa chama cha upinzani na kuwataka kuendelea kukipa uungwaji mkono hadi uchaguzi mkuu.
Akiongea siku ya Jumatatu kwenye hafla ya kumpigia debe mgombeaji wa chama cha upinzani William Mtengo katika eneo bunge la Malindi, Odinga alisema kuwa serikali ya Jubilee imeshindwa kuwapa imani wakazi na kuwakumbuka tu nyakati za siasa.
Kiongozi huyo aliisuta serikali ya Jubilee kwa kukosa kupigana na visa vya ufisadi ambavyo vimekita mizizi kwa siku za hivi karibuni, na kusema kuwa ataendelea kuwawajibisha viongozi hao kuona kuwa maono yote yanafanikishwa.
Viongozi wengine ambao waliandamana na kiongozi huyo akiwemo Gavana wa Mombasa Hassan Joho na viongozi wengine wa chama hicho kutoka eneo la Pwani waliyasuta madai yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa Jubilee kuhusiana na vyeti vya mgombeaji wa chama hicho.
Kiongozi huyo wa chama cha upinzani atakuwa katika eneo la Pwani kwenye shughuli mbali mbali za kisiasa ikiwemo kampeni za eneo la Malindi na kupigia debe chama chake kabla ya uchaguzi mkuu ujao.