Kinara wa Cord Raila Odinga amewataka wapiga kura huko Malindi kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura mgombea wa muungano huo Willy Mtengo.
Odinga alionyesha matumaini ya chama cha ODM kupata ushindi katika uchaguzi huo ambao utaandaliwa mwezi ujao, iwapo wananchi watawaunga mkono na kupiga kura kwa wingi.
Akihutubia halaiki ya wananchi waliokuwa kando mwa barabara kuu ya Malindi Lamu siku ya Jumatatu, Odinga alitoa ujumbe wa kuungana kwa kabila zote zilizoko eneo bunge la Malindi ili kutoa tofauti za kisiasa.
Aidha, aliwasihi wakazi kuungana kwa pamoja na kujitolea kumchagua mgombea wa ODM, hatua aliyoitaja kuongeza idadi ya wabunge wa Cord katika bunge la kitaifa.