Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Ziara ya Rais Uhuru Kenyatta mkoani Pwani inazidi kuwatia tumbo joto viongozi wa upinzani, na sasa kinara wa Cord Raila Odinga, amejitokeza na kuipinga kauli ya wadadisi wa kisiasa kuwa ziara hiyo huenda ikayumbisha uungwaji mkoni wa upinzani mkoani humo.

Akiwahutubia wanahabari mjini Nairobi siku ya Jumanne muda mchache baada ya mahakama kuitupilia mbali kesi iliyokuwa ikimkabili seneta wa Bungoma Moses Wetangula, Raila, amesema Pwani itasalia kua ngome ya Cord hata Rais akiendelea kupiga kambi huko.

"Hata kama Uhuru atakaa Mombasa kwa mwaka mmoja, nitahitaji siku moja tu kupata uungwaji mkono," alisema Raila.

Aidha, Raila anadai kuwa Rais Kenyatta anatumia ziara yake Pwani kujipigia debe kisiasa badala ya kuyatekeleza maendeleo na miradi itakayowafaidi wakazi.

Rais amekua akiyatekeleza majukumu yake akiwa katika Ikulu ya Mombasa tangu Desemba 24, ambapo amefanya miradi mbalimbali mjini humo ikiwemo kutoa hati miliki kwa takribani maskwota 5,000 wanaoishi katika shamba la Waitiki.

Hata hivyo, ziara yake imeshuhudia ukosoaji kutoka kwa mrengo wa upinzani, huku gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho, akimlaumu kwa kutomfahimisha kuuhusu ujio wake mjini humo.

Haya yanajiri wakati Cord na Jubilee zinajitayarisha kumenya katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Kilifi ambao umeratibiwa kufanyika Machi 7, mwaka huu.

Tayari Cord imemtua Willy Baraka Mtego kukiwania kiti hicho kilichobaki wazi baada ya aliyekuwa mbunge Dan Kazungu, kuteuliwa waziri wa madini na Rais Kenyatta mwezi Desemba mwaka jana.