Viongozi wa kisiasa kaunti ya Kilifi na wadau wa sekta ya elimu sasa wanamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha kuwa mzozo uliopo baina ya walimu na tume ya SRC unasuluhishwa.
Mbunge wa Magarini Harison Gharama Kombe amesema kuwa ni jambo la kuhuzunisha kuona walimu wakiendelea kuhangaikia swala la nyongeza ya mishahara kila uchao bila ya mafanikio.
Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano na wadau wa sekta ya elimu mjini Mombasa siku ya Jumapili, Kombe amesema ni wakati sasa Rais Kenyatta kuchukua hatua dhabiti na kusuluhisha tatizo hilo ili walimu kupata haki yao.
“Tunamwomba Rais wetu kuingilia kati hili swala la mzozo wa TSC na Knut kuhusu mishahara ili kuwasaidia wanafunzi kutokumbwa na changamoto za kielimu na kufanya vyema katika mitihani ya kitaifa,” alisema Kombe.
Wakati uo huo amekionya chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini Knut kukoma kuzozana na tume ya kuajiri walimu nchini TSC kuhusu swala la mishahara na badala yake kuandaa mazungumzo ya kina na tume ya SRC.