Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kampeni zinaendelea kupamba moto katika eneo bunge la Malindi siku chache kabla uchaguzi mdogo kufanyika ambapo wakaazi wa eneo hilo wanatarajiwa kumchagua mbunge mpya.

Kiti hicho cha ubunge kiliachwa wazi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Dan Kazungu kuwa waziri mpya wa madini.

Sasa upande wa upinzani umejitokeza na kutaja uteuzi huo wa Kazungu kama mbinu tu ya kujitafutia umaarufu katika eneo la Pwani.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka anayewakilisha upinzani alisema kuwa uteuzi huo hauna manufaa yoyote kwa wapwani.

Akiongea huko Likoni, Kaunti ya Mombasa siku ya Jumapili, Kalonzo alisema kuwa mbinu ya Jubilee ya kuwashawishi viongozi wa upinzani kwa kuwapa kazi ni ya kisiasa na wala sio ya manufaa kwa Wakenya.

“Walienda wakamnyakua mjumbe wetu wa Cord Dan Kazungu huko Malindi wakamuingiza Jubilee eti wanampa kazi ya kuchimba madini,” alisema Kalonzo.

Wakati huo huo, Kalonzo aliongeza kuwa Cord itafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa mbinu ya Jubilee ya kutafuta uungwaji mkono eneo hilo inadidimia.

Alisema kuwa ziara ndefu ya Rais Kenyatta katika eneo la Pwani na pia kutembelea maeneo ya Malindi ilionyesha wazi kwamba alikuwa akiwashawishi wakaazi.

“Alikuja akakaa huku akazungumza na watu wa Pwani lakini mimi nasisitiza kwamba Malindi ni ngome ya Cord,” aliongeza Kalonzo.

Tangu Dan kazungu kuteuliwa kama waziri wa madini, upande wa serikali pamoja na ule wa upinzani umeonekana kuchukua fursa hiyo kujitafutia umaarufu kwenye kampeni hizo za ubunge.

Katika uchaguzi huo mdogo wa tarehe Machi 7, chama cha ODM kilimteua Willy Mtengo kama mwaniaji wa kiti hicho huku Jubilee ikimteua Philip Charo ambapo wawili hao wanapigiwa upato zaidi.