Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya wafuasi wa Jubilee na wafanyibiashara mjini Eldoret wamepongeza hatua ya rais Uhuru Kenyatta kualika viongozi wa upinzani katika mkutano baina ya kiongozi wa Kanisa la Katoliki duniani Papa Francis na rais Ikulu.

Hatua hiyo imetajwa kama ya hekima na ya kuonyesha kujitolea kwa rais Uhuru kuunganisha Wakenya wa matabaka yote bila mapendeleo.

Kwa mujibu wa Mlezi wa Chama cha Jubilee North-Rift Bw Joseph Wainaina ni kwamba rais Kenyatta ameonyesha ukamavu kwa kualika kinara wa Cord Bw Raila Odinga na viongozi wengine wa kisiasa katika mkutano huo wa Ikulu.

“Rais wetu ameiga unyenyekevu wa Papa kwa kualika upinzani ikulu, hii ndio tabia ambayo kila kiongozi nchini anapaswa kuiga,” alisema Bw Wainaina.

Bw Wainaina alitaka wanasiasa alikwa kutumia nafasi hiyo kuonyesha umoja wa Wakenya na kuombea umoja kote nchini wala wasitumie fursa hiyo kuendeleza ajenda yao ya kisiasa.

Msimamo sawa na huo ulitolewa na afisa anayehusika na maswala ya ugatuzi katika muungano wa Cord Bw Kipkorir arap Menjo ambaye alisema kama upinzani wamekumbatia fursa hiyo ili kuonyesha kwamba Papa si mgeni wa Jubilee tu bali ni mgeni wa Wakenya wote.

Wakati huo huo Bw Wainaina amesifu mabadiliko ambayo rais Kenyatta alifanyia baraza lake la mawaziri kwa kusema kuwa mabadiliko hayo yatachangia kwa kina kukabiliana na ufisadi na kurejesha hadhi ya utawala wa Jubilee.

"Kile tunataka kwa sasa ni kuona Wakenya wakiunga mkono hatua hiyo mbali na kuhakikisha kuwa kila mtu anajibika ili kukabiliana na ufisadi nchini," alisema.