Rais Uhuru Kenyatta amesema vita dhidi ya dawa za kulevya vitafanikiwa iwapo watalengwa walanguzi wakuu wa mihadarati.
Akizungumza na vijana kutoka Pwani katika ikulu yake ya mjini Mombasa siku ya Jumatano, Rais Uhuru alisema licha ya hilo, serikali itajenga vituo katika Kaunti ya Lamu na Mombasa ili kuwasaidia mateja kuwachana na uraibu.
Kwenye mkutano huo, Rais Uhuru aliwataka vijana kushirikiana na serikali kutafuta suluhu ya matatizo yanayowakabili.
Vijana katika ukumbi huo walipewa fursa ya kumuuliza maswali rais, ambapo mengi yaliangazia zabuni za vijana, wanawake na walemavu, ambapo rais alisema atachukua hatua kwa wizara ambazo zitakuwa hazitengi asilimia 30 ya zabuni kwa ajili ya makundi hayo.