Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa Wakenya pamoja na viongozi wa dini kuiombea nchi ya Kenya dhidi ya adui mkubwa wa usalama wa nchi.

Rais Kenyatta amesema kuwa sharti kila mmoja awe katika nafasi ya kuiweka nchi hii na ulimwengu kwa jumla kwenye maombi kwa kulaani vitendo vya magaidi, pamoja na wahalifu wengine wanaohatarisha usalama wa nchi.

Kenyatta aliahidi kuwa serikali yake itaendelea kufanya bidii na kujitolea ili kuona wananchi wako salama na wanaendesha shughuli zao bila hofu yoyote.

Akiwahutubia zaidi ya waumini elfu moja katika kanisa kuu la katholiki la Holy Ghost Cathedral lililoko mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Kenyatta aliwatakia Wakenya wote heri njema ya kusherehekea siku kuu ya Krismasi na kuwapongeza viongozi wa makanisa kwa juhudi za kudumisha neno na kuhubiri amani miongoni mwa wakenya.

“Tunapoendelea kusherehekea Krismasi, tusisahau kuiombea nchi. Nawatakia sherehe iliyo na fanaka na mwaka wa 2016 ulio wa baraka na maendeleo. Mungu awabariki na abaraiki Kenya,” alisema Kenyatta.

Rais Uhuru alikuwa ameandamana na mkewe na watoto wake kusherehekea siku kuu ya Krismasi katika ikulu ya Mombasa.