Share news tips with us here at Hivisasa

Rais Uhuru Kenyatta pamoja na gavana wa Mombasa Hassan Joho walizindua rasmi ujenzi wa barabara ya Port Reitz itakayounganisha uwanja wa ndege wa Moi na bandari ya Mombasa.

Mradi huo unaokadiriwa kugharimu takriban shilingi bilioni 2 unatarajiwa kuinua pakubwa biashara ukanda wa Pwani na nchi nzima kwa ujumla, na pia kuimarisha sekta ya utalii.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo siku ya Jumamosi mjini humo, Rais Kenyatta alisema kuwa mradi huo utakapokamilika utawavutia zaidi wawekezeji wa kimataifa kuja humu nchini.

“Hii ni njia moja ya kuinua biashara hapa nchini, na huu sio mradi wa Kenya peke yake bali Afrika Mashariki na hata pia utalii utaimarika zaidi,” alisema Rais.

Kwa upande wake gavana Joho alipongeza hatua hiyo na kusema kuwa kupitia ushirikiano wa kaunti yake na serikali kuu watahakikisha kuwa Wapwani wanafaidi kupitia ujenzi huo.

“Huu ni ushirikiano wa serikali ya Mombasa, serikali kuu pamoja na wathamini kutoka mataifa ya nje. Tunaamini kuwa tutasaidia kupunguza msongomano wa watu na magari unaoshuhudiwa kila siku eneo hili,” alisema Joho.

Aidha Rais alisema kuwa kuna takribani shilingi bilioni 2.5 zilizotengwa kwa kuwafidia wale wote waliyoondolewa katika makaazi yao ili kupeana nafasi kwa ujenzi huo.

Waziri wa uchukuzi James Macharia pia alihudhuria hafla hiyo ambapo pia viongozi hao waliahidi kushughulikia suala la barabara ya Mariakani na Dongo kundu.

Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo ya Port Reitz umefadhiliwa na serikali ya uingereza kwa ushirikiano na serikali ya Kenya.