Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nyamira Alice Chae amemwomba Rais Uhuru Kenyatta kutokubali kuondoa wanajeshi kutoka nchi jirani ya Somalia.
Hii ni baada ya baadhi ya viongozi na wapinzani wake kumwomba Rais kuwaondoa wanajeshi ili kupunguza maafa ya wanajeshi hao.
Kulingana na Chae, ikiwa serikali ya Kenya itawaondoa wanajeshi wa KDF kutoka nchi hiyo, basi huenda Kenya itangazwe kuwa nchi ambayo imeogopa kupambana na vita kati ya kundi la Al shabaab na wanajeshi nchini Somalia.
Akizungumza siku ya Jumanne mjini Nyamira, Chae aliomba Rais Kenyatta kutofuata yale wapinzani wake wanamzinikisha kuondoa wanajeshi wa KDF na kuomba kuwa wanajeshi hao waendelee kupambana na kundi hilo la Al shabaab nchini Somalia hadi wasalimu amri.
“Naomba Rais wetu Kenyatta kutokubali kuwaondoa wanajeshi wa KDF nchini Somalia hadi tushinde vita vinavyoendelea kati ya KDF na kundi la al shaabaab,” alisema Chae.
Aidha, Chae aliomba wakenya kuendelea kuomba wanajeshi wa KDF wanaoendelea kupambana na kundi la uhalifu la Al shabaab nchini Somalia na kuomba wakenya wote kuishi kwa amani kila wakati.
“Naomba wakenya tujiunge pamoja kwa maombi ili tuweke wanajeshi wetu katika mikono ya Mungu ili nao waweze kushinda vita nchini Somalia,” aliongeza Chae.