Baraza kuu la Wazee wa Kaya eneo la Pwani limeshinikiza rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati mizozo ya ardhi ya Pwani na kutafuta suluhu la kudumu ili kuzuia kufurushwa kwa wenyeji.
Kulingana na Mwenyekiti wa Baraza hilo Erustus Mrira Kubo, katiba inamuangazia vyema mwananchi kuwa na hati miliki ya ardhi anayoishi lakini cha kustajabisha idadi kubwa ya wakazi wa Pwani hawana hati miliki za ardhi zao na kuchangia kufurushwa kwa wenyeji na wanyakuzi wa ardhi.
Akiwahutubia wakazi wa Utanga huko Kisauni siku ya Jumanne, Bw Kubo alisema kwamba hatua hiyo imechangia kukithiri kwa mizozo ya ardhi huku akimtaka rais Kenyetta kulizuia Bunge la kitaifa kutoivunjilia mbali tume ya kitaifa ya ardhi kwani jamii ya wapwani ina imani na Tume hiyo.
"Wakati umefika sasa wakuona kwamba swala la ardhi eneo la pwani linatatuliwa na tunamhimiza Rais wetu kututambua kama wazee wa kaya na kuchukua jukumu lake kikatiba kama Rais na kulitatua swala la ardhi," alisema Bw Kubo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ardhi ya Barawa huko Kisauni Joyce Riziki aliishtumu serikali ya kaunti ya Mombasa kwa kuwavunjia nyumba zao pamoja na kuwafurusha katika ardhi ya Barawa iliyo na zaidi ya wakazi 470 na kuachwa bila makao, japo akamshinikiza Rais Kenyetta kuingili kati mzozo huo.
"Tunamuomba mheshimiwa Rais kuingilia kati tatizo la uskwota eneo la Pwani na kutoa hati miliki za ardhi kwa jamii ya wapwani ili swala la uskwota lisitishwe," alisema Bi Riziki.