Rais Uhuru Kenyatta aliwaongoza maafisa wa usalama nchini katika shughuli ya kuyazindua magari mapya yatakayotumiwa na maafisa wa polisi kuwakabili magaidi.
Akizungumza siku ya Jumanne wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika makao makuu ya maafisa wa kupambana na ghasia GSU mjini Nairobi, Rais Kenyatta alisema kuwa magari hayo ya kivita yatatumika katika mipaka ya Kenya ili kuimarisha usalama wa nchi.
Aidha, rais alisema kuwa kuzinduliwa kwa magari hayo ni hatua mojawapo yanayolenga kuborosha huduma inayotolewa na maafisa wa polisi kwani sasa hawatayategemea tena magari ya jeshi kama ilivyokua hapo awali.
“Kama serikali lengo letu kuu ni kuhakikisha kuwa usalama wa wananchi wetu unakua imara. Ili kufanikisha hilo, lazima tuboreshe idara yetu ya usalama,’’ alisema Rais Kenyatta.
Wakati wa uzinduzi huo, rais aliyafanyia majaribio magari hayo yenye uwezo wa kuwabeba watu 30.
Magari hayo yaliletwa nchini siku ya Jumamosi, majuma mawili tangu Rais Kenyatta kutoa ahadi kua serikali itawapa maafisa wa polisi nchini magari mapya ya kuvikabili visa vya uhalifu na ugaidi.