Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzindua rasmi mradi wa taa za mitaani hii leo, Ijumaa katika uwanja wa Makadara mjini Mombasa. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kwa mjibu wa msemaji wa Ikulu ya Rais, Manoah Esipisu, Kenyatta tayari amezuru baadhi ya mitaa mjini humo ambapo alikagua na kuthibitisha kukamilika kwa uwekaji wa taa hizo. 

''Tayari ametembea mtaani hapa usiku kwa mguu na kuhakiki kwamba mradi umekamilishwa, Ijumaa itakua tu kuuzindua,'' alisema Esipisu. 

Kulingana na mkurugenzi wa kampuni ya umeme nchini Ben Chumo, mradi huo umeigharimu serikali kuu shilingi milioni 380, na sasa serikali za kaunti zitahitajika kulipa bili ya matumizi ya kila mwezi. 

Mradi huo ambao umetekelezwa katika Kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale unalenga kuimarisha ukuaji wa uchumi kwa kuwawezesha wafanyibiashara kuendesha shughuli zao saa 24 kwa siku pamoja na kuimarisha usalama. 

Maafisa wa serikali kuu pamoja na viongozi wa kisiasa akiwemo Gavana wa Mombasa Hassan Joho, mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na seneta wa Nairobi Mike Sonko wanatarajiwa kuhudhuria shughuli hiyo.