Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuondoka eneo la Pwani siku ya Alhamisi baada ya kupiga kambi katika kaunti sita za eneo hilo zaidi ya wiki tatu.
Kulingana na habari kutoka ikulu ndogo ya rais ya Mombasa ni kuwa rais anatarajiwa kuenda jiji kuu la Nairobi ili kuweza kushughulikia masuala kadhaa ambayo yanalenga nchi, suala moja kuu likiwa usalama na mashambulizi ya wanajeshi wa KDF Ijumaa iliyopita.
Awali ziara ya rais ilikuwa imeratibiwa kuenda kwa wiki mbili, lakini kutokana na sababu na miradi mingi ambayo alihitaji kufanikisha na kuzindua ilimbidi rais kuongeza ziara yake kwa awamu mbili kwa faida ya wakazi wa kaunti mbali mbali za pwani.
Katika ziara hiyo, kaunti ya Lamu iliweza kufaidi miradi ya barabara pamoja na maji, huku Kaunti ya Mombasa ikishuhudia kuzinduliwa kwa miradi mitatu imara ikiwemo ile ya mradi wa mwangaza mitaa maarufu kama ‘Washa Umeme Mtaani’ pamoja uzinduzi wa barabara ya kupanua uchukuzi wa shehena kutoka bandari kuu ya Mombasa.
Rais anaondoka huku kukiwa na wito kwa serikali yake kuwatoa wanajeshi wa Kenya kutoka nchi ya Somalia ili kuwanusuru na mashambulizi ambayo mara nyingi yamechangia maafa ya raia wengi pamoja na waweka usalama hao.