Wawaniaji wa viti vya ubunge katika uchaguzi mkuu ujao eneo la Mlima Elgon wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwakumbuka wenyeji wa eneo hilo na kuwapa vyeti miliki vya mashamba.
Wakiongeamjini Nakuru Jumatano wakati walihutubia jamii ya Elgon inayoishi mjini Nakuru, mwaniaji Peter Kibet Sirai aliyeongoza wengine alisema kwamba wakazi hao wamekuwa wakidhulumiwa kwa muda mrefu ambao wameishi eneo hilo kama maskwota, licha ya kuwa kwenye ardhi yao, na itakuwa wametendewa haki wakipata hati miliki.
Akisisitiza kuwa Mlima Elgon ni eneo bora katika ukulima, Kibet alisema kwamba wakipewa hati miliki, wakaazi hao watapata afueni ya kupewa mikopo kwenye benki na kufanya kilimo.
“Vile ambavyo rais amemaliza mgogoro wa shamba la Waitiki, vivyo hivyo ndivyo amalize hujuma ya kihistoria dhidi ya jamii yetu ya eneo la Mlima Elgon,” alisema Kibet.
Kibet anapania kupigania ubunge wa eneo la Mlima Elgon, na atamenyana na mbunge wa sasa John Serut.