Mamlaka ya umeme mashinani REA, inatarajia kutia sahihi makubaliano na Wizara ya Maji ili kuhakikisha kuwa shule ambazo zimenufaika na umeme zinaweza kupata fursa ya kupokea maji safi ili kutoa huduma bora kwa wanafunzi katika shule hizo.
Akizungumza mjini Nakuru siku ya Ijumaa, mwenyekiti wa mamlaka hiyo Simon Gicharu alidokeza kuwa idadi kubwa ya shule za msingi nchini zimepokea huduma hizo za umeme.
Alisema kuwa mamlaka ya REA iko katika harakati za mwisho kukamilisha jukumu lao ili shule ambazo bado hazijafikiwa ziweze kunufaika na bidhaa hiyo muhimu.
"REA na Wizara ya Maji tayari zimeweka mikataba ya makubaliano ambapo katika kipindi cha siku tatu, tutakuwa tumetia sahihi ili kuhakikisha kuwa shule zote za humu nchini ambazo tayari zimewekwa nguvu za umeme, zinapata pia maji safi ya kunywa, kwa minajili ya kuimarisha masomo na pia huduma bora kwa wanafunzi," Alisema Bw Gicharu.
Gicharu alisema kuwa utumizi wa rasilimali ambayo haiwezi kutumika tena (non-renewable energy) nchini iko chini kwa asilimia moja.
Alisema kuwa mamlaka hiyo inanuia kuimarisha kiwango chake katika kipindi cha miaka mitano ijayo, hususan katika utumizi wa nguvu za miyale ya jua, na hivyo kupunguza gharama ya maisha nchini.